Dkt. Noha El-Mekkawy: Safari ya Kifikra na Uongozi Katikati ya Mageuzi ya Kisiasa na Maendeleo katika Mashariki ya Kati

Dkt. Noha El-Mekkawy: Safari ya Kifikra na Uongozi Katikati ya Mageuzi ya Kisiasa na Maendeleo katika Mashariki ya Kati

Imetafsiriwa na: Reem Ehab 
Imehaririwa na: Mervat Sakr 
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr 

Katika dunia inayoshuhudia mabadiliko makubwa ya kisiasa na kijamii, viongozi wenye maono makubwa na dhamira thabiti ya kuleta mabadiliko chanya hujitokeza. Miongoni mwao ni Dkt. Noha El-Mekkawy, Mkuu wa Chuo cha Masuala ya Kimataifa na Sera za Umma (GAPP) katika Chuo Kikuu cha Amerika kilichoko Kairo, ameyekuwa mstari wa mbele kama sauti ya kielimu na kitaalamu inayounga mkono mageuzi na uongozi bora katika eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

Katika safari yake ya kitaaluma na kitaalamu, El-Mekkawy ametoa mchango mkubwa katika kuunda mikakati ya maendeleo jumuishi, sambamba na juhudi za kuendeleza uwezeshaji wa wanawake, kuongeza mshikamano wa kijamii, na kusisitiza thamani ya haki ya kijamii. Kadhalika, ameshiriki kwa nafasi ya pekee katika majukwaa ya kimataifa, akiwakilisha sauti ya Kiarabu katika Umoja wa Mataifa na katika vituo mbalimbali vya tafiti duniani.

Amefanikiwa kuchanganya uzoefu wa kielimu na utekelezaji wa vitendo, jambo lililomfanya kuwa mfano wa kipekee wa uongozi wa kifikra na wa kivitendo kwa pamoja. Yeye hakuishia kwenye uchambuzi na nadharia pekee, bali ameacha alama kupitia programu na mipango inayolenga kujenga taasisi zenye uadilifu na ufanisi zaidi.

Hadithi ya Dkt. Noha El-Mekkawy si historia ya kitaalamu pekee, bali pia ni ushahidi hai wa uwezo wa mwanamke wa Kiarabu kushiriki kwa dhati katika kuunda mustakabali bora wa eneo hili, na kuchangia kupitia uzoefu na maono yake katika kujenga dunia yenye haki na utu zaidi.