Dkt. Yasmin Moussa: Sauti ya Kisheria ya Misri katika Majukwaa ya Kimataifa
Imetafsiriwa na: Omar Bahauddin
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Katika nyanja za diplomasia ya kisheria na kwenye majukwaa ya mahakama za kimataifa, jina la Dkt. Yasmin Moussa linaonekana miongoni mwa akili bora za kisheria zinazoiwakilisha Misri kwa kujiamini na kwa uwezo mkubwa.
Akiwa mshauri wa kisheria katika Ofisi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Moussa anachukua jukumu muhimu katika kuunda misimamo ya kisheria ya Misri mbele ya taasisi za kimataifa, na anawakilisha mfano bora wa mwanamke Mmisri katika nyanja za sheria na diplomasia.
Sehemu muhimu katika safari yake ni pamoja na kuiwakilisha Misri mbele ya mahakama na vyombo mashuhuri vya kimataifa kama vile Mahakama ya Haki ya Kimataifa (ICJ) na Mahakama ya Kimataifa ya Sheria ya Bahari (ITLOS). Pia, ni mwanachama wa kudumu wa Mahakama ya Usuluhishi ya Kudumu (PCA), jambo linalomweka katika nafasi ya uongozi katika kiwango cha sheria za kimataifa.
Kabla ya kuchukua nafasi yake ya sasa, Dkt. Yasmin Moussa alihudumu kama mshauri wa masuala ya kisheria na kibinadamu katika Ujumbe wa Kudumu wa Misri kwenye Umoja wa Mataifa huko Geneva. Aidha, ameshika nafasi mbalimbali katika Wizara ya Mambo ya Nje ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Waziri, Ofisi ya Naibu Waziri, Idara ya Kisheria, na Idara ya Masuala ya Pande Nyingi.
Athari zake za kielimu zimeenea hadi vyuo vikuu mashuhuri, ambapo amefundisha sheria za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Marekani cha Cairo, Chuo Kikuu cha Cairo, pamoja na St Edmund’s College na Magdalene College katika Chuo Kikuu cha Cambridge.
Katika upande wa utafiti wa kisayansi, yeye ndiye mwandishi wa kitabu mashuhuri “Competing Fundamentalisms and Women’s Family Rights in Egypt” kilichochapishwa na wachapishaji wa kimataifa Brill. Aidha, tafiti zake zimechapishwa katika majarida muhimu ya sheria za kimataifa kama vile British Yearbook of International Law, International and Comparative Law Quarterly, International Review of the Red Cross, na Cambridge International Law Journal, ambacho alihudumu kama mhariri mkuu wake mwaka 2012–2013.
Dkt. Moussa ana historia tajiri ya kielimu: ana shahada ya kwanza katika Sayansi ya Siasa na Uchumi na shahada ya Uzamili wa Sheria za Haki za Binadamu za Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Marekani cha Cairo, shahada ya kwanza ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Cairo, shahada ya uzamili katika sheria za kimataifa kutoka London School of Economics, na shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge.
Dkt. Yasmin Moussa anawakilisha hadithi ya mafanikio ya kipekee ya mwanamke Mmisri ambaye ameunganisha ubora wa kitaaluma na uzoefu wa kivitendo wa hali ya juu, na kwa hekima na weledi wake amechangia kuimarisha uwepo wa Misri wa kisheria na kidiplomasia katika anga ya kimataifa