Ahmed Mokhtar: Kiongozi Mbadilikaji Anayeunda Mustakabali wa Misri Kupitia Mafunzo na Maendeleo
Imetafsiriwa na: Aisha Ramadan
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Katika dunia inayobadilika kwa kasi, hitaji la viongozi wenye ujuzi na uwezo wa kuzoea hali mpya limekuwa muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Ahmed Mohamed Mokhtar anajitokeza kama kiongozi muhimu katika maendeleo ya Misri, akijitoa maisha yake kukuza vipaji na kusukuma mabadiliko chanya na maendeleo kupitia mafunzo, ushauri na huduma za kijamii.
Wasifu wa Mokhtar unaonyesha mtaalamu mwenye vipaji vingi, msingi imara wa elimu, na azimio la kuwawezesha wengine. Ana shahada ya uzamili katika Usimamizi wa Biashara (MBA) kutoka Chuo cha Biashara cha Chuo Kikuu cha Benha, pamoja na shahada ya msingi ya Sheria kutoka Chuo Kiakuu cha Ain Shams. Mafanikio haya ya kitaaluma yameimarishwa na uzoefu mpana wa kazi na mafunzo maalumu.
Kama mhitimu wa Mpango wa Uongozi wa Kitaaluma wa Rais (EPLP) katika Chuo cha Taifa cha Mafunzo (NTA) chini ya uangalizi wa Rais wa Jamhuri, pamoja na kuwa mhitimu wa kundi la pili la Ufadhili wa Nasser wa Uongozi wa Kimataifa, Mokhtar amekuza stadi zake katika nyanja nyingi zikiwemo uongozi, mahusiano ya umma, upangaji mkakati, na usimamizi wa migogoro. Mafunzo haya yamempa uelewa mpana wa changamoto za uongozi wa kisasa na usimamizi wa umma.
Dhamira ya Mokhtar ya kujenga uwezo inaonekana wazi katika nafasi zake kama mhadhiri na mkufunzi katika Chuo cha Taifa cha Mafunzo na Chuo Kikuu cha Ain Shams. Hupatia viongozi chipukizi mafunzo ya stadi binafsi na ujuzi wa kiutawala, huku akishirikiana pia na vijana kupitia mpango maalumu wa chuo kwa watoto.
Mchango wake umeonekana wazi katika kumbi za mihadhara na majukwaa ya mafunzo. Tangu mwaka 2016, amekuwa mshauri na mkufunzi wa Baraza la Utamaduni la Briteni (British Council), ambapo amekuwa nguzo ya kukuza mazungumzo, uraia hai na miradi ya kijamii. Ameunda ushirikiano na taasisi mbalimbali zikiwemo vyuo vikuu, mashirika na jumuiya za vijana, ili kukuza utamaduni wa kuelewana na mshikamano.
Uzoefu wake katika mafunzo na uratibu umejitokeza wazi katika kazi yake na Kampuni ya Misriyati, akilenga ujenzi wa amani, mawasiliano, usuluhishi wa migogoro, na usimamizi wa utofauti. Shauku yake ya kuunda mazingira shirikishi inaonekana katika kazi zake na mashirika kama SiOS, Al-Nidaa, na CARE International, ambako ameshughulikia masuala muhimu kama usawa wa kijinsia, ujumuishaji wa watu wenye ulemavu, na mawasiliano yasiyo ya vurugu.
Kabla ya kuingia kwenye kazi yenye ushawishi wa mafunzo na ushauri, Mokhtar alipata uzoefu muhimu katika sekta ya ndege kama Mkaguzi wa Usalama wa Ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kairo, akionesha uwezo wake wa kushughulikia majukumu magumu na yenye mahitaji makubwa.
Zaidi ya mafanikio yake ya kitaaluma, Mokhtar pia anajihusisha kikamilifu na maendeleo ya kijamii. Aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Kijamii ya mpango wa EPLP na ni mjumbe wa bodi ya Taasisi ya Maameroon kwa Maendeleo ya Jamii. Ushiriki wake katika kamati za asasi za kiraia na kazi za kujitolea ndani ya Baraza Kuu la Vijana, pamoja na kuandaa na kuratibu matukio makubwa kama Kombe la Dunia la Wachezaji wa Vijana (U-20) na mbio za "Misri kwa Ajili ya Tiba", unaonesha kujitolea kwake kwa ushiriki wa kiraia na uwajibikaji wa kijamii.
Safari ya Ahmed Mokhtar ni ushahidi wa nguvu ya elimu, mafunzo na kujitolea. Yeye ni nguvu chanya inayounda mustakabali wa Misri, kiongozi anayeendeleza maendeleo na kuhimiza mazungumzo kupitia mipango na majadiliano mbalimbali.