Sameh Shoukry: Mwanadiplomasia Aliyebeba Sauti ya Misri Katika Ulingo wa Kimataifa
Imetafsiriwa na: Mohaned Galal
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Tangu alipochukua jukumu la Waziri wa Mambo ya Nje mnamo mwaka 2014, kufuatia kuingia madarakani kwa Rais Abdel Fattah Al-Sisi, jina la Sameh Shoukry limeibuka kama miongoni mwa sura kuu za diplomasia ya Misri, akiwa na uzoefu uliojengeka kwa zaidi ya miongo minne katika nyanja za siasa za kigeni, na rekodi ya kujivunia katika kulinda nafasi ya Misri katika kanda na duniani.
Shoukry amezaliwa mnamo mwaka 1952, na kuhitimu kutoka Chuo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Ain Shams. Aliingia katika utumishi wa kidiplomasia mnamo mwaka 1976, akianza safari yake kama afisa mdogo wa kidiplomasia katika Wizara ya Mambo ya Nje. Baadaye alipanda ngazi katika nyadhifa mbalimbali kwenye balozi za Misri nje ya nchi na katika vituo vya kufanya maamuzi nyumbani. Katika kila nafasi aliyoshika, aliacha alama yake kama mwanadiplomasia wa kiwango cha juu, mwenye ustadi wa mazungumzo ya utulivu na uwezo wa kushughulikia masuala magumu kwa uthabiti na uwiano.
Safari yake ya kidiplomasia ilijumuisha miji mikuu mikuu ya dunia na mashirika ya kimataifa. Alifanya kazi London na Buenos Aires, kisha akawa mshauri katika ujumbe wa kudumu wa Misri katika Umoja wa Mataifa mjini New York. Baadaye alishika majukumu nyeti zaidi kama Mkurugenzi wa Idara ya Masuala ya Marekani na Kanada, na Katibu wa Rais wa Jamhuri kwa masuala ya taarifa na ufuatiliaji.
Mnamo mwaka 1999, aliteuliwa kuwa Balozi wa Misri nchini Austria na Mwakilishi wake wa kudumu katika mashirika ya kimataifa mjini Vienna, ambapo alicheza jukumu muhimu katika kuiwakilisha Misri ndani ya Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA), na pia aliongoza kundi la G-77 na China, sambamba na kuiwakilisha nchi yake katika Shirika la Kupiga Marufuku Majaribio ya Nyuklia kwa Jumla (CTBTO). Pia aliongoza timu ya Misri katika mazungumzo ya Mkataba wa Kupambana na Uhalifu Ulioandaliwa Kimataifa huko Vienna mnamo mwaka 2000.
Shoukry alihusiana sana na masuala ya unyakuzi wa silaha, ambapo aliongoza kikao cha maandalizi cha pili cha Mkutano wa Mapitio ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia, na mnamo mwaka 2006 alisimamia uratibu wa muungano wa New Agenda Coalition katika Mkutano wa Kudumu wa Usitishaji Silaha. Hii iliongeza hadhi yake kimataifa kama sauti tulivu lakini thabiti katika masuala ya usalama wa dunia.
Miongoni mwa hatua zake mashuhuri pia ni uwakilishi wake wa Misri kama Balozi mjini Washington (2008–2012), kipindi kilichojaa changamoto nyingi za kikanda na kimataifa. Katika kipindi hicho, alifanikiwa kudumisha njia za mazungumzo ya kimkakati na Marekani, na kueleza kwa uwazi na uwiano msimamo wa Misri.
Baada ya kurejea Kairo, alishika nyadhifa za uongozi ndani ya wizara, hadi alipoteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje mnamo mwaka 2014. Tangu wakati huo, ameongoza diplomasia ya Misri katika hatua nyeti, ikiwa ni pamoja na juhudi za kudumisha uthabiti wa kikanda, kulinda msimamo wa Misri kuhusu bwawa la Renaissance, kushirikiana na mataifa makubwa, na kuiwakilisha Misri katika majukwaa ya kimataifa. Amekuwa akijulikana kwa uwezo wake wa kuunda misimamo ya Misri kwa ufanisi mkubwa, akichanganya uimara na diplomasia tulivu.
Sameh Shoukry ameoa na ana watoto wawili, na hadi leo anaendelea kuwa mfano wa mwanadiplomasia aliyesuguliwa na uzoefu, na kuthibitisha nafasi yake kama mmoja wa walinzi wakuu wa maslahi ya kitaifa katika medani ya kimataifa.