Ashraf Mahmoud: Mwanahabari Aliyebadilisha Mtazamo wa Michezo na Utamaduni katika Ulimwengu wa Kiarabu

Ashraf Mahmoud: Mwanahabari Aliyebadilisha Mtazamo wa Michezo na Utamaduni katika Ulimwengu wa Kiarabu

Imetafsiriwa na: Mohammed Magdy
Imehaririwa na: Mervat Sakr 
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr 

Katika ulimwengu ambapo vyombo vya habari vinagusana na michezo na utamaduni, jina la Ashraf Mahmoud linang’ara kama nguzo kuu ya uandishi wa habari za michezo na utamaduni katika ulimwengu wa Kiarabu. Yeye si mwandishi wa kawaida tu katika gazeti mashuhuri la Al-Ahram, bali ni kinara wa kuimarisha dhana ya utamaduni wa michezo kama kichocheo cha maendeleo na uelewa wa kijamii.

Tangu mwanzo wa safari yake, Mahmoud ameacha alama ya kipekee. Alikuwa mmoja wa waanzilishi wa jarida Al-Ahram Al-Arabi mnamo mwaka 1997, na akahitimisha safari yake humo kwa kuteuliwa kuwa Mhariri Mkuu mnamo mwaka 2012. Mnamo mwaka 2005, alizindua jarida Al-Thaqafa Al-Riyadiyya (Utamaduni wa Michezo), lililobeba maono yake kwamba michezo si mashindano pekee, bali pia ni fikra, malezi na mwanga.
Ndoto zake hazikomei kwenye uandishi wa habari. 

Mnamo mwaka 2011, alianzisha Shirikisho la Kihmisri la Utamaduni wa Michezo, kisha mwaka 2015 akashirikiana kuunda mashirikisho ya Kiarabu na Kiafrika ya Utamaduni wa Michezo, hatua iliyoweka msingi wa taasisi za Kiarabu na Kiafrika zinazounganisha michezo na maarifa. Aidha, amekuwa mwanachama hai wa Shirikisho la Kimataifa la Utamaduni wa Michezo tangu mwaka 2013 hadi sasa.

Katika upande wa uandishi wa moja kwa moja, sauti yake imekuwa ya karibu sana kwa mashabiki wa kandanda kupitia maoni na uchambuzi wake kwenye majukwaa maarufu ya Kiarabu na kimataifa kama vile:
• Televisheni ya Misri, Kituo cha Nile Sports na Radio ya Vijana na Michezo,
• Sauti ya Uswisi ya Kiarabu (tangu 1994),
• Monte Carlo International (tangu 2003 hadi sasa),
• Kituo cha Al-Jazeera Sports, na vilevile vituo vya Abu Dhabi, Al-Mustaqbal na Al-Jadeed vya Lebanon,
• Shirika la Habari la Ufaransa na Umoja wa Vyombo vya Habari vya Kiarabu, ambako amejipambanua kama mchambuzi, mtangazaji na mkufunzi mwenye uwezo mkubwa.

Historia yake katika uandishi wa habari imejaa ushiriki katika mashindano makubwa ya kimataifa: kuanzia Kombe la Dunia Marekani 1994 hadi Olimpiki ya London 2012 na Rio 2016, pamoja na Kombe la Dunia la Vijana na Chipukizi, Kombe la Mataifa ya Afrika, Kombe la Asia na Ghuba, na pia michezo ya Kiarabu na Kiafrika.

Mbali na kipaza sauti na kamera, kalamu yake imeendelea kunawiri. Ameandika vitabu kadhaa vinavyoeleza safari yake na kuchambua uhusiano kati ya michezo na utamaduni, ikiwemo:
• Hadithi kutoka kwenye Uwanja wa Kijani (1991),
• Sanaa ya Uchanganuzi wa Michezo (2010),
• Hatuna Ila Uwanja Mkubwa (2015),
• Kukimbia kwa Maneno: Michezo katika Uwanja wa Fasihi (2022),
• na kitabu chake cha hivi karibuni Utamaduni wa Michezo: Chakula cha Mwili, Elimu ya Akili na Uundaji wa Hisia (2023), kinachojumuisha falsafa yake ya uandishi wa habari na ubinadamu.

Ashraf Mahmoud ni zaidi ya mwandishi wa habari au mchambuzi wa michezo; yeye ni sauti ya mwanga na elimu, aliyefanikiwa kuunganisha kalamu na neno, uwanja na maandiko, dimba na hisia, na kufanya utamaduni wa michezo kuwa mradi wa maisha na ujumbe wa kijamii.