Sahar Al-Jubouri... Muiraqi Anayeongoza Juhudi za Umoja wa Mataifa Kutoka Kairo kwa Ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina
Imetafsiriwa na: Omar El-Dessouky
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Kutoka kwenye korido za Umoja wa Mataifa, jina la Sahar Al-Jubouri limeibuka kama moja ya sauti muhimu za uongozi zinazotetea haki za wakimbizi wa Kipalestina na haki za binadamu katika moja ya migogoro changamano zaidi Mashariki ya Kati.
Akiwa na uzoefu mpana wa Umoja wa Mataifa uliodumu kwa miongo kadhaa, leo Al-Jubouri anaongoza Ofisi ya Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada na Kazi kwa Wakimbizi wa Kipalestina Mashariki ya Karibu (UNRWA) jijini Kairo, akisimamia juhudi za kimkakati za shirika hilo tangu mwaka 2018 na akiratibu msaada wa dharura kwa ajili ya mgogoro wa Gaza kupitia Misri.
Safari ya Al-Jubouri katika kazi za Umoja wa Mataifa ilianza katika mazingira ya baada ya Vita Baridi, akihudumu katika misheni za kulinda amani huko Cambodia, Msumbiji, Haiti na Yugoslavia ya zamani. Uzoefu huu wa moja kwa moja ulimjengea uwezo mkubwa wa kufanya kazi katika mazingira tete zaidi duniani. Baadaye, alihudumu katika Kamati Maalum ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq na Tume ya Uchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa kwa Asia Magharibi (ESCWA), kabla ya kushika nafasi za uongozi katika mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kama Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Madawa ya Kulevya na Uhalifu (UNODC), ambako alisimamia mawasiliano na utetezi, na akaratibu ushirikiano na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu pamoja na Baraza la Mawaziri wa Sheria na Mambo ya Ndani wa Kiarabu.
Hapo awali, alishikilia nyadhifa za juu katika Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) nchini Misri na Iran, na pia alianzisha sekretarieti ya pamoja kati ya shirika hilo na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, jambo ambalo ni mafanikio ya kitaasisi yanayoakisi uwezo wake wa kujenga madaraja kati ya mashirika ya kikanda na ya kimataifa.
Al-Jubouri ana shahada ya uzamili katika Usimamizi wa Biashara za Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha ESLSCA cha Ufaransa, na shahada ya kwanza ya tafsiri kutoka Chuo Kikuu cha Al-Mustansiriya mjini Baghdad, jambo lililompa mchanganyiko wa kipekee wa ujuzi wa lugha na usimamizi katika dunia inayohitaji usahihi na mawasiliano ya kitamaduni mbalimbali.
Leo, Sahar Al-Jubouri anaendelea kuongoza ofisi ya UNRWA mjini Kairo, si tu kama mratibu wa mikakati, bali pia kama sauti thabiti katika kutetea haki ya wakimbizi wa Kipalestina na heshima ya binadamu katika nyakati ngumu zaidi za misukosuko.