Waziri mwenye hadhi ya mwanariadha... Ashraf Sobhy anaunganisha ustadi wa uwanjani na dira ya kimkakati

Waziri mwenye hadhi ya mwanariadha... Ashraf Sobhy anaunganisha ustadi wa uwanjani na dira ya kimkakati

Imetafsiriwa na: Doaa Karam Muhammed 
Imehaririwa na: Mervat Sakr 
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr 

Ukiitazama safari ya Dkt. Ashraf Sobhy, utagundua haraka kuwa unakabiliana na mhusika ambaye amejumuisha uzoefu wa kitaaluma, utaalamu wa michezo, na uongozi wenye ufahamu, hadi kuwa miongoni mwa majina maarufu katika sekta ya vijana na michezo nchini Misri na eneo la Kiarabu.

Dkt. Ashraf Sobhy amezaliwa mwaka 1968, na alianza safari yake ya kitaaluma kwenye zulia la karate, ambapo alipata mkanda mweusi “4 Dan”, na akatwaa ubingwa wa taifa, kabla ya kuanza njia yake katika nyanja za usimamizi na masoko ya michezo, na kuwa mmoja wa wataalamu maarufu katika fani hii kitaaluma na kiutendaji.

Alifuzu kutoka Chuo cha Elimu ya Michezo katika Chuo Kikuu cha Helwan mnamo mwaka 1989 kwa heshima na alama za juu, kisha akapata shahada ya uzamili katika Mahusiano ya Umma na Usimamizi wa Michezo mnamo mwaka 1994, na akaendeleza safari yake ya kielimu kwa kupata shahada ya uzamivu katika Usimamizi wa Michezo kutoka Chuo Kikuu cha Helwan na Chuo Kikuu cha Ottawa cha Kanada mnamo mwaka 2000.

Safari yake ya kikazi ilianza mapema, ambapo alifanya kazi kama mhadhiri wa elimu ya michezo katika Chuo Kikuu cha Helwan, akibobea katika masoko na uwekezaji wa michezo, sambamba na kushika nyadhifa kadhaa za uwanjani, ikiwemo mtaalamu wa shughuli za michezo katika Klabu ya Zamalek, na kocha mkuu na kiongozi wa idara ya karate katika klabu hiyo kati ya mwaka 1994 hadi 1997.

Mnamo mwaka 2000, Sobhy aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa mahusiano ya umma katika Klabu ya Zamalek, na hapo ndipo ikaanza safu ya majukumu ya kiutawala yaliyoongezeka hatua kwa hatua. Aliteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Shirikisho la Soka la Misri mwaka 2004, na pia alitoa ushauri wa kimasoko kwa Wizara ya Vijana na Michezo kwa miaka kadhaa. Alihudumu kama mkurugenzi mtendaji wa Klabu ya Baniyas ya Umoja wa Falme za Kiarabu kati ya mwaka 2009 na 2010, na aliongoza kamati ya masoko ya Mashindano ya Kiarabu ya Vyuo Vikuu. Pia alimwakilisha Klabu ya Zamalek katika Kamati ya Ligi ya Wataalamu mnamo mwaka 2011, kisha akawa mkuu wa sekta ya masoko na uwekezaji katika klabu hiyo hadi mwaka 2012.

Mnamo mwaka 2012, Sobhy alijiunga na Bodi ya Usimamizi wa Uwanja wa Taifa wa Kairo, kisha akawa rais wa mamlaka hiyo hadi mwaka 2014, ambapo alifanikiwa kuubadilisha uwanja huo kuwa kituo cha uwekezaji halisi. Hilo lilimpa nafasi kubwa ya kuteuliwa kuwa msaidizi wa Waziri wa Vijana na Michezo, Khaled Abdel Aziz, katika serikali ya Dkt. Kamal El-Ganzouri tangu Agosti 2014 hadi Machi 2016, kabla ya kujiuzulu akipinga kudharauliwa kwa jukumu lake.

Baada ya kutokuwapo kwenye medani ya kiserikali kwa muda wa miaka miwili, Dkt. Ashraf Sobhy alirudi kwa nguvu mnamo mwaka 2018, akiteuliwa kuwa Waziri wa Vijana na Michezo akichukua nafasi ya Mhandisi Khaled Abdel Aziz. Tangu wakati huo, amefanikisha mafanikio mengi, iwe ni katika kuimarisha miundombinu ya michezo, au katika kuwawezesha vijana na kuzindua mipango ya kitaifa na ya kijamii, kama vile programu za ujasiriamali, makongamano ya vijana, na vituo vya vijana vilivyoboreshwa. Wakati wa uongozi wake, Misri imeshuhudia kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa, sambamba na juhudi dhahiri za kuboresha vituo vya vijana katika mikoa yote, na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya michezo na vijana.

Dkt. Ashraf Sobhy ana mchanganyiko wa kipekee wa uzoefu wa kitaaluma, asili ya michezo, na uwezo wa kiutawala, jambo lililomfanya kuwa mhusika muhimu katika taswira ya michezo na vijana wa Misri katika miaka ya karibuni. Anasifika kwa uwezo wake wa kuunganisha dira ya kimkakati na mawasiliano ya kijamii, katika wakati ambapo taifa la Misri linatazamia kutekeleza kikamilifu nguvu za vijana na kufanikisha maendeleo endelevu.

Vyanzo:
Bawaba ya Al-Ahram ya Misri 
Urais wa Baraza la Mawaziri