Walid Haqiqi: Zaidi ya miaka 30 katika upangaji na usimamizi wa rasilimali za maji nchini Misri
Imetafsiriwa na: Rahaf Mahmoud Mohamed
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Mhandisi Walid Haqiqi ni mojawapo wa wataalamu mashuhuri katika nyanja ya upangaji na usimamizi wa rasilimali za maji nchini Misri, akiwa na uzoefu wa zaidi ya miongo mitatu, ambapo aliweka juhudi zake katika kuandaa sera, mikakati, na mipango madhubuti kwa ajili ya kukuza sekta ya maji tangu mwaka 1998, akichangia kwa namna ya dhati katika kuchora mustakabali wa maji nchini.
Haqiqi amehudumu katika nafasi kadhaa za uongozi ndani ya Wizara ya Rasilimali za Maji na Umwagiliaji ya Misri. Nafasi kuu alizoshika ni pamoja na Mkurugenzi wa Mradi wa Mpango wa Kitaifa wa Rasilimali za Maji, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mageuzi ya Kimuundo, Kisha Mkuu wa Idara Kuu ya Rasilimali na Matumizi ya Maji, na Mkuu wa Idara Kuu ya Tafiti na Utafiti, jambo lililomwezesha kusimamia moja kwa moja mafaili nyeti yanayohusu usalama wa maji wa Misri.
Mbali na kazi yake ya kiserikali, Mhandisi Walid Haqiqi pia amehudumu katika majukumu ya ushauri kwa taasisi kadhaa za kikanda na kimataifa, jambo lililomruhusu kupanua upeo wa uzoefu wake na kufungua njia mpya za ushirikiano katika sekta ya maji. Aidha, aliteuliwa kuwa msemaji rasmi wa Wizara ya Rasilimali za Maji na Umwagiliaji, akiwa sauti ya wizara hiyo katika majukwaa ya habari, makongamano ya kitaifa na ya kimataifa. Hivi sasa, anashikilia wadhifa wa Mkuu wa Kitengo cha Mipango katika Wizara ya Rasilimali za Maji na Umwagiliaji, sambamba na kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Sekretarieti ya Wiki ya Maji ya Kairo, imeyokuwa jukwaa la kimataifa lenye heshima kubwa kwa ajili ya mazungumzo na kubadilishana uzoefu katika sekta ya maji.
Safari ya Walid Haqiqi inawakilisha kielelezo cha kujitolea kitaaluma na dira ya kimkakati katika sekta inayohesabika kuwa miongoni mwa nyeti zaidi na endelevu, huku jina lake likibakia limeunganishwa na kila juhudi inayolenga kuhakikisha usalama wa maji wa Misri na ukanda mzima.