Miral Sabri Al-Ashry: Mwandishi wa habari katika moyo wa mapambano kwa ajili ya uhuru wa vyombo vya habari 

Miral Sabri Al-Ashry: Mwandishi wa habari katika moyo wa mapambano kwa ajili ya uhuru wa vyombo vya habari 

Imetafsiriwa na: Nada Mohammed Fawzi
Imehaririwa na: Mervat Sakr 
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr 

Kutoka kwenye maeneo ya migogoro nchini Libya hadi kwenye kumbi za vyuo vikuu mashuhuri barani Ulaya na Mashariki ya Kati, Dkt. Miral Sabri Al-Ashry anaandika sura za kipekee katika safari inayochanganya uandishi wa habari za uchunguzi, utafiti wa kitaaluma, na utetezi wa uhuru wa vyombo vya habari na usalama wa waandishi wa habari.

Kwa sasa, Miral ni Mkuu wa Kitivo cha Habari na Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha East London, tawi la Kairo lililo chini ya European Universities in Egypt (EUE). Pia anahudumu kama Kiongozi Mwenza wa Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika Kituo cha Uhuru wa Vyombo vya Habari cha Chuo Kikuu cha Sheffield nchini Uingereza, na ni mtaalamu wa kitaaluma katika usalama wa waandishi wa habari katika Chuo Kikuu cha Liverpool. Mbali na hayo, ni mwandishi wa habari aliyesajiliwa anayefuatilia migogoro nchini Libya kwa ajili ya jukwaa la Eurasia Review tangu mwaka 2019.

Al-Ashry alipokea Tuzo ya Taifa kwa Wanawake katika Sayansi ya Kijamii mnamo mwaka 2023, na Tuzo ya Mtafiti Bora katika Mkutano wa Usalama wa Mtandaoni na Usimbaji Data mwaka 2024, kutokana na utafiti wake jasiri kuhusu “Athari za Sheria za Misri kwa Uhuru wa Kupata Taarifa.”

Alipata shahada ya udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Ain Shams kwa heshima ya juu zaidi, na alipanda ngazi katika taaluma kutoka mhadhiri msaidizi hadi kuwa profesa kamili. Alifundisha katika vyuo vikuu mashuhuri kama Chuo Kikuu cha Amerika mjini Cairo na Chuo Kikuu cha Future, ambapo alishika nafasi za juu za kitaaluma na kiutawala, zikiwemo “Naibu Mkuu wa Kitivo” na “Mkuu wa Idara ya Habari za Kisiasa.” Alichunguza na kusimamia tasnifu kadhaa za kielimu na kushiriki katika maandalizi ya mikutano muhimu, ikiwemo: “Misri katika Dunia Inayobadilika”, “Uandishi wa Habari za Kisayansi za Kiarabu katika Enzi ya Vyombo vya Habari vya Kidijitali”, na “Jumhuri Mpya: Kuelekea Mustakabali Bora.”

Tangu mwaka 2019, Al-Ashry amefuatilia matukio na mafaili kadhaa yenye moto nchini Libya, Syria na Yemen, na ameandika makala za uchambuzi zinazoshughulikia ugumu wa jiopolitiki katika eneo hilo. Pia alijitokeza kwa kutoa uchambuzi makini wa mwingiliano kati ya teknolojia, vyombo vya habari na siasa, hasa katika zama za akili bandia.

Al-Ashry amechapisha zaidi ya makala 28 yaliyopitiwa na wataalamu katika majarida ya kimataifa yaliyokadiriwa (Q1 na Q2), pamoja na vitabu 6 vya kitaaluma vilivyoshughulikia masuala ya uhuru wa kujieleza, maadili ya vyombo vya habari, usalama wa kidijitali, na mageuzi ya kidijitali katika vyombo vya habari vya Kiarabu. Hivi sasa anashiriki katika tafiti za kimataifa kwa ushirikiano na taasisi kama Kituo cha Mafunzo ya Kistratejia NESA na Chuo cha Kijerumani cha DW Akademie.

Mbali na mafanikio yake ya kielimu, Miral anaongoza mtandao wa wahitimu wa DW katika eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, ambapo anaratibu mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu usalama wa kidijitali, uandishi wa habari za uchunguzi, na uendelezaji wa mitaala ya vyuo vikuu. 

Al-Ashry anawakilisha mfano wa mwanamke wa Kiarabu anayeweza kuchanganya ukali wa kitaaluma, uadilifu wa kitaalamu, na mchango wa kijamii kwa ajili ya vyombo vya habari huru na vyenye uwajibikaji.