Dkt. Mostafa Madbouly: Mhandisi Aliyeiongoza Misri Kuelekea Mageuzi Makubwa
Imetafsiriwa na: Mohamed El-Sayed Ahmed
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Katika kipindi muhimu katika historia ya Misri ya kisasa, Rais Abdel Fattah El-Sisi alimteua Dkt. Mostafa Kamal Madbouly kuunda serikali ya Misri mnamo tarehe Juni 7, 2018, akichukua nafasi ya Mhandisi Sherif Ismail, na kuwa Waziri Mkuu katika moja ya hatua nyeti zaidi zilizohitaji uwiano kati ya ujenzi na mageuzi, maendeleo na upangaji wa muda mrefu.
Dkt. Madbouly amezaliwa mwaka 1966, na alihitimu katika Kitivo cha Uhandisi, Chuo Kikuu cha Kairo mnamo mwaka 1988 akibobea katika usanifu wa majengo. Baadaye aliendeleza safari yake ya kielimu iliyong'ara ambapo alipata shahada ya Uzamili katika upangaji wa miji kutoka Chuo Kikuu cha Kairo mnamo mwaka 1992, stashahada ya masomo ya juu katika usimamizi wa maendeleo ya miji kutoka Taasisi ya Rotterdam nchini Uholanzi mnamo mwaka 1993, kisha shahada ya Uzamivu (PhD) katika usanifu wa majengo (mwelekeo wa upangaji wa miji) mnamo mwaka 1997, kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Kairo na Chuo Kikuu cha Karlsruhe nchini Ujerumani.
Safari yake ya kielimu haikuwa tu mwanzo, bali ikawa daraja la taaluma ndefu katika taasisi za kitaifa na kimataifa. Alipanda vyeo katika taasisi ya upangaji wa miji kuanzia makamu wa rais hadi mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo. Baadaye akawa Mkurugenzi wa Taasisi ya Mafunzo na Utafiti wa Miji, kisha Mkurugenzi wa Kikanda wa nchi za Kiarabu katika Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa UN-Habitat kuanzia 2012 hadi 2014, ambapo alipata uzoefu mkubwa wa kimataifa katika maendeleo ya miji endelevu.
Mnamo mwezi Februari 2014, Dkt. Madbouly aliteuliwa kuwa Waziri wa Makazi, Huduma na Maendeleo ya Miji. Katika wadhifa huu alisimamia mageuzi makubwa katika sekta ya makazi nchini Misri, akizindua miradi mikubwa ya kitaifa ikiwemo mradi wa makazi ya kijamii, mji mkuu mpya wa kiutawala, na miji ya kizazi cha nne, jambo lililomfanya ajulikane kama “Mhandisi wa upanuzi wa kisasa wa miji ya Misri”.
Jina lake halikuondoka katika ulingo wa uongozi wakati wa nyakati nyeti. Rais El-Sisi alimkabidhi jukumu la Kaimu Waziri Mkuu mnamo mwezi Novemba 2017 wakati Waziri Mkuu wa wakati huo alikuwa akipokea matibabu, jambo lililotazamwa kama maandalizi ya kuteuliwa kwake rasmi miezi michache baadaye.
Tangu kuchukua madaraka mnamo mwaka 2018, Dkt. Madbouly ameendeleza mageuzi ya kiuchumi, ameimarisha ajenda za ulinzi wa kijamii, kuboresha mazingira ya uwekezaji, na kupanua miradi ya kitaifa. Pia ameongoza nchi katika nyakati za changamoto, kama janga la virusi vya Korona na athari za vita vya Urusi na Ukraine katika uchumi wa Misri.
Ametoa kipaumbele kwa kuboresha miundombinu, kukuza usafiri wa kisasa na kuendeleza mabadiliko ya kidijitali, hatua zilizoongeza uwezo wa taifa kukabiliana na mabadiliko ya dunia na kuimarisha nafasi ya Misri katika ripoti za maendeleo za kimataifa.
Dkt. Madbouly anajulikana kwa mtazamo wake wa kupanga unaounganisha hali halisi na fursa za baadaye. Hii inaonekana wazi katika mwelekeo wa serikali katika kujenga miji mipya, kuboresha vijiji vya Misri, programu ya “Maisha Bora”, na miradi ya maendeleo yenye athari za kijamii na kiuchumi.
Anasalia kuwa mfano wa kiongozi mtaalamu aliyefanikisha kuhamisha ujuzi wake kutoka kwenye mihadhara ya vyuo na taasisi za upangaji hadi nafasi ya juu ya uongozi wa kitaifa, akiacha alama katika historia ya sasa ya Misri na kuunda sura ya mustakabali wake.