Ahmed Rizk: Safari ya Kitaaluma katika Kuendeleza Viwanda na Ushirikiano wa Kimataifa
Imetafsiriwa na: Maryem Salama
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Tangu kuanza kwa taaluma yake mnamo mwaka 2004, Ahmed Rizk ameonesha mafanikio makubwa katika uwanja wa uchumi na maendeleo ya viwanda, na kujijengea nafasi kama mtaalamu mashuhuri wa sera za maendeleo ya kiuchumi na ushirikiano wa kimataifa. Baada ya kuhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Kairo, Kitivo cha Uchumi na Sayansi ya Siasa, alianza kazi yake kama mtafiti wa uchumi katika Kituo cha Utafiti na Mafunzo ya Uchumi na Fedha (CEFRS), ambako alishiriki katika tafiti kuhusu masuala ya uchumi wa ndani na wa kimataifa.
Mnamo mwaka 2018, Ahmed Rizk alijiunga na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) kama Afisa wa Programu ya Kitaifa katika Ofisi ya Kanda ya Misri. Katika jukumu hili, alihusika katika kusukuma maendeleo endelevu ya viwanda nchini na katika kanda. Mnamo mwaka 2022 alipandishwa cheo na kuwa Naibu Mwakilishi wa Kanda, akichukua jukumu la kubuni sera na programu za kimkakati zinazounga mkono sekta ya viwanda na kukuza ushirikiano wa kimataifa.
Rizk anashikilia Shahada ya Uzamili katika Masomo ya Ulaya na Mediterania kutoka Chuo Kikuu cha Kairo, pamoja na Stashahada ya Juu ya Biashara ya Kimataifa kutoka Taasisi ya Biashara ya Nje ya Uingereza. Katika zaidi ya miaka 15 ya kazi, amejipatia uzoefu mkubwa katika kuongeza tija na kusimamia miradi mbalimbali katika sekta ya maendeleo ya viwanda.
Ana ujuzi mpana wa kiufundi katika tafiti za soko, mipango ya kuuza nje, mikakati ya maendeleo, na programu za mageuzi ya kiuchumi. Aidha, ameimarisha mahusiano thabiti na taasisi za serikali, mashirika ya kimataifa, na programu zinazofadhiliwa na washirika wa maendeleo.
Kazi ya Ahmed Rizk ni mfano wa kujitolea na uthabiti katika kuendeleza sera za viwanda na uchumi nchini Misri, hali inayomuweka kama mmoja wa wataalamu wenye heshima kubwa katika fani yake.