Koshari: Hazina ya Kimsri na Mafanikio ya Kimataifa ya Koshari Abu Tarek
Imetafsiriwa na: Shahd Ashraf
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Koshari Abu Tarek ni miongoni mwa migahawa inayojulikana zaidi duniani kwa kuandaa chakula cha jadi cha Misri kijulikanacho kama koshari. Ni mlo wa wananchi unaoakisi utambulisho wa chakula cha Kimsri kwa karne nyingi.
Asili ya koshari inarudi maelfu ya miaka, hadi enzi za ustaarabu wa Misri ya kale. Wamisri wa wakati huo walikuwa wakila dengu lililopikwa, njegere, ngano na vitunguu pamoja na kitunguu saumu. Baadaye wali ulichezwa nafasi muhimu, sambamba na mchuzi wa nyanya, na ndipo ikazaliwa aina ya koshari tunayoifahamu leo.
Historia ya familia ya Koshari Abu Tarek inaanza takribani miaka 95 iliyopita, walipoanza kuuza koshari mitaani katika Kairo ya kifalme. Walianza kwa kutumia sanduku la kioo walilolibeba kichwani na kutembea nalo mitaani. Kufikia miaka ya 1940, gari maarufu la koshari lilibuniwa, na hadi leo bado lipo karibu na mgahawa wao katikati ya jiji la Kairo, ambapo koshari huendelea kutolewa.
Mgahawa wa Koshari Abu Tarek umeorodheshwa miongoni mwa taasisi bora zaidi 1% duniani kwa mujibu wa tovuti ya TripAdvisor, na pia umeingizwa kwenye orodha ya migahawa 100 bora zaidi duniani kwa mujibu wa TasteAtlas. Mnamo mwaka 2015, mgahawa huu ulipata umaarufu zaidi baada ya kuandaa sahani kubwa zaidi ya koshari duniani, tukio lililoingia rasmi katika Guinness World Records.
Leo hii, mgahawa wa Abu Tarek katikati ya Kairo unawakaribisha wageni mashuhuri, wakiwemo mawaziri na watu maarufu wa kimataifa. Mwaka 2025, serikali ya Misri iliwasilisha rasmi ombi kwa Shirika la UNESCO ili koshari isajiliwe kama urithi wa kitamaduni wa Misri.