Kituo cha Jeshi la Wanamaji cha Alexandria: Alama ya Kijeshi Inayoakisi Nguvu na Historia Tukufu ya Jeshi la Majini la Misri
Imetafsiriwa na: Wafaa Khaled El.said
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Katikati ya Bahari ya Mediterania, kwenye pwani ya jiji la kihistoria la Alexandria, lipo moja ya vituo vya kijeshi vya zamani na vikubwa zaidi katika Mashariki ya Kati. Hii ndiyo Kambi ya Jeshi la Wanamaji ya Alexandria, moyo wa meli za kivita za Misri, ngome thabiti ya usalama wa baharini wa taifa, na nguzo imara katika kukabiliana na changamoto za kikanda.
Historia ya Kambi ya Alexandria inarejea kipindi cha kabla ya Mapinduzi ya Julai 23, 1952, wakati Misri ilikuwa ikianza safari yake kuelekea uhuru kamili. Tangu wakati huo, kambi hii imepitia maboresho endelevu yaliyoiweka katika nafasi ya kipekee kama moja ya kambi muhimu zaidi za kijeshi katika eneo.
Kwa miongo kadhaa ya maendeleo ya kimfumo, imekuwa kituo cha kimkakati cha shughuli za uendeshaji, mafunzo, na ulinzi wa Jeshi la Wanamaji la Misri katika Bahari ya Mediterania.
Miaka ya karibuni imeshuhudia hatua kubwa za kihistoria katika upanuzi wa kambi hii. Miongoni mwa maendeleo hayo ni ujenzi wa kizuizi cha mawimbi cha urefu wa kilomita tano, kilichopanua eneo la kambi kwa zaidi ya asilimia 127. Hatua hii imeongeza nafasi ya kupokea vitengo vipya vya majini na kuimarisha miundombinu ya uendeshaji, ikithibitisha dhamira ya Misri kujenga jeshi la wanamaji la kisasa lenye uwezo wa kulinda maslahi ya taifa na kufanikisha ulinzi wa kikanda.
Kituo hiki kimewekewa vifaa vya hali ya juu vinavyohusisha:
• Gati kubwa kwa ajili ya kupokea meli za kijeshi na kibiashara za ukubwa wowote.
• Kituo cha mafunzo ya wanamaji chenye mabwawa ya kuigiza vita kwa usahihi wa juu.
• Karakana ya manowari yenye mifumo ya kisasa ya matengenezo na mafunzo.
• Mfumo wa usambazaji na uhifadhi wa silaha unaoongeza uwezo wa mapambano ya vikosi vya majini.
• Mnara wa kumbukumbu wa askari asiyejulikana, ukikumbuka sadaka za mashujaa wa jeshi la wanamaji la Misri.
Hivi karibuni, kituo hiki kilipokea meli ya kivita “Al-Qahhar” ya daraja la MEKO-A200, mojawapo ya meli za kivita za kisasa zenye matumizi mengi duniani. Hatua hii inaonesha mwendelezo wa jitihada za Misri kusasisha silaha na teknolojia kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa baharini.
Kituo cha Alexandria kina jukumu muhimu katika:
• Kulinda pwani za Misri na kuhakikisha usalama wa njia za baharini na anga.
• Kutoa mafunzo ya hali ya juu kwa maafisa na wanamaji.
• Kutumikia na kutengeneza meli na manowari kwa ufanisi mkubwa.
• Kutoa msaada wa vifaa na lojistiki kwa vikosi vilivyoko baharini.
Ndani ya kumbi za kituo, picha, sanamu na medali zinahifadhi kumbukumbu za historia ya mapambano ya wanamaji wa Misri kuanzia vita vya kale hadi changamoto za sasa, na kutoka mashujaa wa Vita ya Oktoba hadi ulinzi wa Bahari ya Mediterania.
Kwa hakika, Kituo cha Jeshi la Wanamaji cha Alexandria siyo tu jengo la kijeshi. Ni alama ya kitaifa inayoonyesha safari ya Misri kuelekea nguvu kamili ya kijeshi, msingi wa ulinzi wa kikanda, na ujumbe wa wazi kwamba Misri iko salama baharini, ikilinda maji yake kwa uaminifu na nguvu.