Kituo cha Kimataifa cha Kairo... Nguzo ya Misri ya kuimarisha amani na kujenga utulivu barani Afrika na duniani
Imetafsiriwa na: Youssef Mohamed
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Nchini Misri, hususan mjini Kairo, tangu mwaka 1994, Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ilizindua mpango mahsusi uliolenga kuanzisha Kituo cha Kikanda cha Kairo cha Usuluhishi wa Migogoro na Udumishaji wa Amani barani Afrika. Lengo lilikuwa kujenga taasisi ya kitaaluma na kiutendaji inayounga mkono juhudi za amani na usalama katika bara la Afrika. Hakikuwa kituo cha mafunzo ya tukio moja pekee, bali kimekua kwa kasi katika kipindi cha miaka, kikidhihirisha nafasi muhimu ya Misri katika eneo na katika medani za kimataifa.
Mnamo mwaka 2017, mageuzi makubwa yalifanyika wakati Azimio la Waziri Mkuu namba 1396 lilipotolewa. Azimio hili lilikipa kituo hicho hadhi ya kisheria, na kulibadilisha jina kuwa “Kituo cha Kimataifa cha Kairo cha Usuluhishi wa Migogoro, Udumishaji na Ujenzi wa Amani.” Kituo sasa kiko chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri, na madhumuni yake yamepanuka kwa kiwango cha kikanda na kimataifa, yakiwajumuisha hasa nchi za Afrika, Kiarabu na Kiislamu.
Kazi za kituo hiki haziishii tu katika kuandaa mafunzo, semina na makongamano, bali pia zinahusisha tafiti za kimkakati, ukuzaji wa sera, na ujenzi wa uwezo wa watu binafsi na taasisi katika nyanja za amani na usalama, hususan katika nchi zilizotoka kwenye mizozo. Kituo kinajivunia kuwa kimeendesha zaidi ya mafunzo 300, kikiwafunza zaidi ya washiriki 30,000 kutoka nchi 96, zikiwemo nchi 50 za Afrika, na hivyo kukifanya kuwa mojawapo ya vituo vikubwa vya mafunzo katika eneo hili.
Kituo kinaendesha shughuli zake kupitia programu kuu nane, zinazoshughulikia masuala muhimu ya kisasa, yakiwemo:
• Udumishaji na ujenzi wa amani
• Kuzuia msimamo mkali na ukatili unaosababisha ugaidi
• Wanawake, amani na usalama
• Vijana, amani na usalama
• Upunguzaji wa silaha, uondoaji wa wanajeshi na ujumuishaji wao tena katika jamii (DDR)
• Vitisho vya kuvuka mipaka
• Mabadiliko ya tabianchi, amani na maendeleo
Kila programu inawakilisha majibu thabiti kwa changamoto zinazojitokeza katika mfumo wa kimataifa, na inaonesha juhudi za kituo kutoa mafunzo na tafiti zinazofuatilia mageuzi ya kikanda na kimataifa.
Katika utekelezaji wa programu zake, kituo kinafanya kazi kwa karibu na wizara mbalimbali za Misri, hususan Wizara ya Ulinzi na Wizara ya Mambo ya Ndani, pamoja na ushirikiano wa kimataifa unaojumuisha Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na washirika wa maendeleo. Ushirikiano huu unaimarisha ushawishi wa kituo na kupanua upeo wa shughuli zake.
Kituo cha Kimataifa cha Kairo kinajitahidi kutoa programu zake kwa lugha mbalimbali, na kuandaa ziara za uhamasishaji katika nchi kadhaa za Afrika, kikisisitiza dhamira yake ya kushirikiana moja kwa moja na jamii zinazolengwa, na kupanua ushirikiano wake ili kuhusisha wadau wa kikanda na wa kimataifa katika nyanja za amani na usalama.
Kwa wale wanaopenda kufahamu zaidi kuhusu shughuli za kituo, maeneo ya kazi na miradi yake ya baadaye, wanaweza kutembelea tovuti rasmi: www.cccpa-eg.org
Kituo cha Kimataifa cha Kairo siyo tu taasisi ya mafunzo, bali ni mwakilishi wa dhana ya Misri ya kuunga mkono utulivu wa kikanda na kujenga amani ya kudumu. Ni mfano halisi wa uwezo wa Misri wa kuchanganya diplomasia, utaalamu na uongozi wa kitaaluma kwa ajili ya bara la Afrika na dunia kwa ujumla.
Chanzo: Tovuti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri