Kutoka Moyo wa Kidiplomasia Hadi Kilele cha Siasa: Hadithi ya Muhammad Al-Arabi

Kutoka Moyo wa Kidiplomasia Hadi Kilele cha Siasa: Hadithi ya Muhammad Al-Arabi

Imetafsiriwa na: Eman Khalil Zakaria
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Katika mandhari ya siasa za kigeni za Misri, jina la balozi Mohamad E-Orabi linajitokeza kama mojawapo ya nyuso maarufu za kidiplomasia zimezoshiriki katika kuunda sura ya siasa za kigeni za Misri kwa miongo kadhaa. Yeye ni waziri wa zamani wa mambo ya kigeni wa Misri, na mwanadiplomasia ambaye maisha yake yalipita kati ya miji mikuu ya kimataifa, akichora mistari ya mawasiliano kati ya Misri na ulimwengu.

Muhammad Al-Arabi amezaliwa tarehe Januari 26, 1951, na alihitimu katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Kairo mnamo mwaka 1975, akiwa na shahada katika Usimamizi wa Biashara. Mwaka uliofuata, 1976, alijiunga haraka na huduma ya kidiplomasia ya Misri, ambapo alianza safari yake ambayo ingedumu zaidi ya miongo minne katika uwanja wa siasa za kimataifa.

Al-Arabi alihudumu katika miji mikuu muhimu zaidi ya kimataifa; alifanya kazi katika balozi za Misri nchini Kuwait, Uingereza, Marekani, Israel na Ujerumani. Pia alishikilia wadhifa wa katibu maalumu wa Dkt. Boutros Boutros-Ghali, kisha kuwa msemaji rasmi wa Wizara ya Mambo ya Kigeni wakati wa uongozi wa Dkt. Ismat Abdel-Meguid.

Mnamo mwaka 2011, alifikia kilele cha kazi yake ya kidiplomasia alipoteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Misri kwa kipindi kifupi lakini muhimu, kilichokuja katika moja ya hatua nyeti zaidi ambazo nchi ilipitia baada ya Mapinduzi ya Januari.
Pia alikuwa na mchango wa bunge ulioonekana, ambapo aliongoza Kamati ya Mambo ya Kigeni ya Baraza la Wawakilishi la Misri mwaka 2016, akiwa mbunge kati ya mwaka 2015 na 2020, pamoja na nafasi yake ya zamani kama kiongozi wa Chama cha Mkutano.

Balozi Al-Arabi hakujizuia kwenye nyadhifa rasmi pekee, bali aliendelea kushiriki kikamilifu katika nyanja za fikra na diplomasia baada ya kustaafu rasmi. Leo anashikilia nafasi kadhaa za juu, zikiwemo:
• Mwenyekiti wa Baraza la Misri la Mambo ya Kigeni
• Mwenyekiti wa Kituo cha Shaf kwa Masomo ya Baadaye na Uchambuzi wa Mizozo
• Mwenyekiti wa Shirika la Ushirikiano wa Mataifa ya Afrika na Asia
• Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Kituo cha Kistratejia na Mafunzo ya Kanda
• Mwanachama wa Jumuiya ya Sayansi ya Misri
• Mwanachama wa Baraza la Ushauri la Jarida la Siasa ya Kimataifa
• Mwanachama wa bodi kadhaa za uongozi za vyuo na vituo vya utafiti, ikiwemo Kituo cha Utafiti wa Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha Ain Shams, Maktaba ya Kitaifa ya Misri, Mamlaka ya Maonyesho na Mikutano, Chuo Kikuu cha Badr, Chuo Kikuu cha Mfalme Salman, Chuo Kikuu cha Baadaye, Chuo Kikuu cha Uingereza na Chuo Kikuu cha Al-Ahram cha Kanada.

Al-Arabi pia anajitahidi kuhamasisha uzoefu wake kwa vizazi vipya kupitia mihadhara mbalimbali, hasa mfululizo wa mihadhara katika diplomasia ya umma katika Taasisi ya Utamaduni wa Kidiplomasia ya Chuo Kikuu cha Humboldt – Berlin, mojawapo ya vyuo vikuu vya zamani zaidi vya Ujerumani.

Kama ishara ya kuthamini safari yake ya kidiplomasia na mchango mkubwa alioutoa katika kuimarisha uhusiano kati ya Misri na Ujerumani wakati alipohudumu kama balozi mjini Berlin, Mohamad E-Orabi alitunukiwa Medali ya Msalaba Mkubwa wa Daraja la Kwanza kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, mojawapo ya medali za heshima za juu zaidi zinazotolewa kwa wahusika wa kimataifa.