Meja Jenerali Osama Abdel Hamid Mohammed Dawood, Afisa wa Makao Makuu: Safari ya Uongozi na Uaminifu

Meja Jenerali Osama Abdel Hamid Mohammed Dawood, Afisa wa Makao Makuu: Safari ya Uongozi na Uaminifu


Imetafsiriwa na: Farah Mahmoud 
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Ndani ya jeshi la ulinzi la Misri, Kamanda wa Vikosi vya Ulinzi wa Umma na Kijeshi, Meja Jenerali Osama Abdel Hamid Mohammed Dawood, anajitokeza kama kiongozi mashuhuri wa kijeshi, akiwa na rekodi yenye mafanikio makubwa na shahada za kitaaluma na kimkakati za juu.

Rekodi yake ya kipekee inajumuisha sayansi ya kijeshi na kibiashara, ambapo alipata shahada ya kwanza katika sayansi za kijeshi kutoka Kitivo cha Kijeshi na shahada ya kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Helwan. Hivyo, alikuwa na mtazamo wa kina na uwezo wa kusimamia rasilimali kwa ufanisi. Aliendeleza masomo yake ya kitaaluma na kupata shahada ya uzamili katika sayansi za kijeshi, pamoja na cheo cha “Afisa wa Makao Makuu” kutoka Kozi ya Jumla Na. 56.

Uongozi wake ulionekana zaidi kupitia kozi za juu za kijeshi, ikiwemo kozi ya viongozi wa kampuni za kijeshi, kozi ya viongozi wakuu wa vikosi, Kozi ya Maandalizi ya Awali Na. 15 katika Chuo cha Juu cha Kijeshi, Ushirika wa Kitivo cha Vita (Kozi Na. 40), Ushirika wa Kitivo cha Ulinzi wa Taifa cha Sudan (Kozi Na. 30), na Kozi ya Maendeleo ya Ujuzi wa Viongozi Wakuu Na. 4 katika Chuo cha Nasser.

Amewahi kushika nafasi muhimu za uongozi, kama vile: Kamanda wa Kikosi 101 cha Walinzi wa Mipaka ya Pwani, Mkuu wa Makao Makuu ya Vikosi vya Walinzi wa Mipaka, Mkuu wa Kitengo cha Operesheni cha Uongozi wa Walinzi wa Mipaka, Kamanda wa Walinzi wa Mipaka ya Jeshi la Pili, Naibu Kamanda wa Vikosi vya Walinzi wa Mipaka, na hatimaye Kamanda wa Vikosi vya Ulinzi wa Umma na Kijeshi. Nafasi hizi zimempa uzoefu mkubwa katika operesheni za kijeshi, ulinzi wa mipaka, na usalama wa taifa.

Uzoefu wake pia ni wa kimataifa, akiwa amewakilisha Misri nchini Pakistan kama Afisa Mshikizi, kushiriki ziara za mafunzo nchini Ufaransa, na kutekeleza majukumu ya usalama wa bandari na pwani nchini Marekani. Pia alipata udhamini kutoka Kitivo cha Ulinzi wa Taifa cha Sudan.

Kwa mchango wake, Meja Jenerali Dawood amepokea medali na tuzo nyingi, ikiwemo: Tuzo ya Huduma Bora, Tuzo ya Wajibu wa Kijeshi (Daraja la Kwanza), Medali ya Operesheni Kamili ya Sinai, Medali ya Juni 30, Medali ya Jubilei ya Fedha kwa Uhuru wa Sinai, Medali ya Huduma Ndefu na Kielelezo Bora (Daraja la Kwanza), Medali ya Jubilei ya Dhahabu ya Ushindi wa Oktoba, Medali ya Jubilei ya Dhahabu ya Mapinduzi ya Julai, na Medali ya Januari 25 ya 2011.

Safari ya Meja Jenerali Osama Abdel Hamid Mohammed Dawood ni mfano wa kiongozi wa kijeshi aliyeunganisha elimu, uongozi na uaminifu wa taifa. Yeye ni kiongozi anayewatia moyo wengine na alama ya kujitolea na uaminifu, akitupa fahari na heshima kupitia dhabihu na mchango wake katika huduma ya taifa.