Abdel Hakim Abdel Nasser... mhandisi aliyeubeba urithi wa uongozi na akaichagua njia ya kazi tulivu

 Abdel Hakim Abdel Nasser... mhandisi aliyeubeba urithi wa uongozi na akaichagua njia ya kazi tulivu

Imetafsiriwa na: Eman Nasser
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr

Katika kitovu cha mji mkuu wa Misri, hususan katika jimbo la Giza, amezaliwa tarehe Januari 8, 1955 Abdel Hakim Gamal Abdel Nasser, mwana wa tano wa kiongozi mashuhuri marehemu Gamal Abdel Nasser, mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa katika historia ya kisasa ya Misri, ulimwengu wa Kiarabu na bara la Afrika. Licha ya kuzaliwa katika familia ya uongozi na mapambano ya kitaifa, Abdel Hakim aliamua kujijengea njia yake ya kitaaluma imara katika uhandisi na sekta binafsi, akichanganya urithi wa kizalendo na kazi ya vitendo.

Abdel Hakim alihitimu kutoka Kitivo cha Uhandisi, Chuo Kikuu cha Kairo, mnamo mwezi Julai 1976, akibobea katika uhandisi wa ujenzi. Mojawapo ya hatua za kwanza baada ya kuhitimu ilikuwa kutumikia jeshi la Misri katika huduma ya taifa kuanzia Septemba 1976 hadi Novemba 1977, kipindi ambacho nchi ilikuwa inajiandaa kwa hatua ya ujenzi upya kufuatia ushindi wa Oktoba wa kihistoria.

Kuanzia mwaka 1979 hadi 2018, Abdel Hakim Gamal Abdel Nasser alianza safari ndefu ya kazi katika sekta ya ukandarasi na uhandisi wa ujenzi, ambapo alijijengea taaluma iliyotengwa mbali na siasa, akipendelea mafanikio ya kivitendo badala ya umaarufu wa kisiasa. Kupitia mtazamo wake wa kitaalamu na uzoefu wa muda mrefu, alishiriki katika utekelezaji wa miradi mikubwa mingi, na akawa mfano wa mhandisi Mmisri anayefanya kazi kwa bidii, kimya kimya, akijenga bila kutafuta sifa.