Dkt. Ali El-Hefnawy aandika: Kuhusu Siku ya Wanawake

Imetafsiriwa na: Noran Ahmed Mohammed saeed
Imehaririwa na: Mervat Sakr
Mratibu wa Lugha ya Kiswahili: Mervat Sakr
Mnamo mwaka 1995, wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Umoja wa Mataifa, shirika hilo lilitangaza kuwa watu wa Mosuo ni miongoni mwa jamii bora na zenye amani zaidi duniani. Watu hawa, wanaokadiriwa kuwa kati ya 30,000 na 60,000, wanaishi katika miteremko ya milima ya Himalaya, kusini-magharibi mwa China. Hebu tujaribu kuelewa ni nini kilichowafanya watu hawa kuwa bora na wenye amani kiasi hiki, kiasi kwamba dunia ikakubaliana na tangazo hili la kipekee.
Mfumo wa kijamii wa watu wa Mosuo ni tofauti na ile ya jamii nyingine duniani kwa maelfu ya miaka. Hii ni jamii ambamo mwanaume hana mamlaka makubwa, na ambapo wanawake ndio wanaoongoza familia. Hizi ni baadhi ya sifa bainifu za jamii hii:
• Mwanamke ndiye mkuu wa familia na ndiye anayefanya kazi zote.
• Hakuna mfumo wa ndoa wa kimila kati ya wanaume na wanawake.
• Mwanamke huishi katika nyumba ya mama yake maisha yake yote, na huchukua uongozi wa familia baada ya kifo cha mama.
• Ili kuhakikisha kuendelea kwa kizazi, wasichana baada ya kubalehe huwapokea vijana wa kiume katika chumba maalum ndani ya nyumba ya mama, bila majukumu ya kifedha au kijamii. Mwanamke anaweza kuzaa na wanaume tofauti, na mwanaume hana haki ya kumiliki mwanamke. Kwa hivyo, hakuna hisia za wivu au umiliki.
• Watoto wa kiume na wa kike huishi katika nyumba ya mama, na hawana uhusiano wa karibu na baba zao, ambao mara nyingi hawawatambui watoto wao.
• Mjomba (yaani kaka wa mama) huchukua nafasi ya baba, akishirikiana na mama katika malezi ya watoto.
• Hakuna migogoro ya urithi, kwani urithi hubaki ndani ya familia na hurithiwa na wanawake pekee. Mama mkubwa ndiye anayefanya maamuzi yote, na mali haibadilishi familia kwa njia ya ndoa.
• Mwanamke ndiye mzalishaji mkuu katika jamii hii, akifanya kazi nyingi ndani na nje ya nyumba. Mwanaume, bila kujali umri wake, hubaki chini ya uangalizi wa mama yake, na husaidia tu katika kazi za kilimo anapoombwa. Hivyo, mwanaume huwa kama chombo cha uzazi tu.
• Serikali ya China ya kikomunisti haikufanikiwa kutekeleza sera ya mtoto mmoja katika jamii hii, kwa kuwa hakuna mfumo rasmi wa familia unaotegemea ndoa.
• Dini ya watu wa Mosuo iko karibu na Ubuddha, na maandishi yao yanafanana na maandishi ya hieroglyph.
Hivyo basi, watu wa Mosuo hawajawahi kushuhudia vita, migogoro au ugomvi katika historia yao yote ndefu, na hawajui hisia za chuki, wivu, wala udhibiti. Hata hivyo, inaonekana kuwa kuingia kwa teknolojia ya kisasa kumeanza kubadilisha mila na desturi zao.
Tuna somo la kutafakari na kuzingatia katika mfano huu wa kipekee wa kibinadamu, enyi wanaume.